Alhamisi 11 Juni 2026 - 20:15
Ujerumani Yazuia Kuwekewa Vikwazo Mawaziri wa Israel ndani ya Umoja wa Ulaya

Hawza/ Wakati baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinataka kuwekewa mawaziri wawili wenye misimamo mikali katika serikali ya Israel, Ujerumani imezuia kufikiwa kwa mwafaka kutokana na upinzani wake, na kwa mara nyingine imejitokeza kuwa miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa Tel Aviv dhidi ya hatua za kinidhamu za Umoja wa Ulaya.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Shirika la Habari la Anadolu, katika kikao cha hivi karibuni cha Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Ulaya (COREPER), suala la uwezekano wa kuweka vikwazo dhidi ya mawaziri wawili wa serikali ya Israel, yaani Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani, na Bezalel Smotrich, Waziri wa Fedha wa utawala huo, lilijadiliwa.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, Ujerumani katika kikao hicho ilitaka orodha ya vikwazo ipunguzwe na kumlenga Ben-Gvir pekee, huku ikisisitiza kwamba; Smotrich asijumuishwe katika orodha hiyo. Aidha, Jamhuri ya Czech ndiyo nchi pekee mwanachama wa Umoja wa Ulaya iliyopinga hata kuwekwa kwa vikwazo dhidi ya Ben-Gvir.

Baadhi ya nchi za Ulaya, zikitegemea matamshi na misimamo ya mawaziri hao wawili wakati wa vita vya Ghaza, zinataka kuchukuliwa hatua kama vile kupigwa marufuku kusafiri na kufungiwa mali zao, hata hivyo, tofauti za maoni kati ya wanachama wa Umoja wa Ulaya bado zinaendelea.

Shada Islam, mtaalamu mwandamizi wa masuala ya Ulaya, katika mahojiano na Shirika la Habari la Anadolu alisema kwamba; Ujerumani daima imekuwa na msimamo wa tahadhari na wa kuzuia dhidi ya hatua yoyote madhubuti ya kuongeza shinikizo kwa Israel.

Alikumbusha kwamba; Ujerumani hapo awali pia ilikuwa imezuia kusimamishwa kwa makubaliano ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Israel mnamo mwezi Aprili.

Mtaalamu huyo huku akirejelea misimamo ya Johann Wadephul, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, alisema kwamba; Berlin ni miongoni mwa nchi zinazozuia Umoja wa Ulaya kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya Israel.

Kwa mujibu wake, nchi kama Ireland, Poland, Ufaransa na Uholanzi zinaunga mkono kuwekwa kwa vizuizi kama marufuku ya kusafiri dhidi ya Ben-Gvir na Smotrich, lakini upinzani wa Ujerumani umezuia kufikiwa kwa uamuzi wa pamoja katika ngazi ya Umoja wa Ulaya.

Shada Islam anaamini kwamba; uungaji mkono mkubwa wa Ujerumani kwa Israel taratibu umeanza kuigharimu Berlin kisiasa na kidiplomasia katika medani ya kimataifa, hasa katika mahusiano yake na nchi zinazojulikana kama “Global South” (Nchi za Kusini mwa Dunia).

Alisisitiza kuwa: "Sera hii imeisababishia Ujerumani gharama kubwa za kidiplomasia." Pia alirejelea kushindwa kwa hivi karibuni kwa Ujerumani kupata kiti kisicho cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kusema kwamba; baadhi ya maafisa wa Ujerumani wamekubali kuwa sera za Berlin kuhusu Israel huenda zilikuwa na athari katika namna nchi mbalimbali zilivyopiga kura.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, kutokana na misimamo yake kuhusu matukio ya Ghaza, Ujerumani inazidi kujikuta katika hali ya kutengwa zaidi katika ngazi ya kimataifa.

Shada Islam aliendelea kueleza kwamba; sera ya Ujerumani kuhusu Israel ina mizizi katika hisia ya wajibu wa kihistoria unaotokana na kipindi cha Utawala wa Nazi na tukio la Holocaust, jambo ambalo limekubaliwa kwa upana barani Ulaya.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba; wajibu huo wa kihistoria haupaswi kugeuzwa kuwa chombo cha kuzuia uwajibikaji kuhusu matukio ya sasa.

Alisema: "Wajibu unaotokana na Holocaust ni ukweli ambao lazima ukubaliwe, lakini kuugeuza kuwa ngao ya kudumu inayozuia uwajibikaji mbele ya janga la karne ya ishirini na moja kunapingana na mafunzo ambayo Ulaya inadai kuwa imejifunza kutokana na historia yake."

Tume ya Ulaya mnamo Novemba 2025, kufuatia ukosoaji kuhusu ukimya wake wa muda mrefu dhidi ya vita vya Ghaza, ilipendekeza kusimamishwa kwa sehemu ya makubaliano ya ushirikiano na Israel pamoja na kuwekwa kwa vikwazo dhidi ya baadhi ya mawaziri wa mrengo wa kulia wa serikali hiyo.

Hata hivyo, kutokana na kutokuwepo kwa mwafaka kati ya nchi wanachama, mapendekezo hayo hayakutekelezwa, na baada ya kuanzishwa kwa usitishaji vita, kwa vitendo yaliwekwa kando.

Mwezi uliopita pia, katika mkutano usio rasmi wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, suala la kumwekea Ben-Gvir vikwazo lilijadiliwa tena, lakini uamuzi wa mwisho ukaahirishwa hadi mkutano rasmi wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya uliopangwa kufanyika tarehe 15 Juni.

Hata hivyo, majadiliano ya awali yaliyofanyika ndani ya COREPER pia hayakuweza kuondoa tofauti zilizopo kati ya wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha